Tuesday, August 30, 2011

MAGOFU YA KILWA, KIVUTIO KWA WATALII

Magofu ya Kilwa ni kivutio kwa watalii.
Na Aisha Mbaga
Magofu ya kumbukumbu ya kihistoria, ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yanayofanyiwa ukarabati yanatarajiwa kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea eneo hilo kutoka ndani na nje ya nchi mara baada ya ukarabati kukamilika.
Mradi huo, unaendeshwa kwa pamoja na serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, nchi ya Ufaransa, Japan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni, Elimu na Sayansi (UNESCO).
Mradi huu wa maendeleo umepania kuinua utalii katika eneo hilo la lililopo kilomita 300 kusini mwa Dar es salaam.
Meneja mradi Bw.John Kimaro anasema kuwa kwa kutangaza eneo la kumbukumbu la magofu la Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kutawaelimisha wengi ambao hawajapata taarifa hizo kwa undani.
Katika ukarabati huo maeneo yanayoshughulikiwa ni pamoja na jumba la kale la Gereza “Gereza Fort” lilojengwa na Wareno mwaka 1505 na kufanyiwa ukarabati upya na Waarabu mwaka 1807,ambalo limeshawekewa umeme “security light” unaotumia nishati ya jua “solar power”.
Magofu mengine yanayofanyiwa ukarabati katika eneo hilo lenye kilomita za mraba 2000 ni Husuni Kubwa yenye eneo la mita za mraba 3000 iliyojengwa karne ya 14 na Husuni Ndogo, Jumba la Makutani “ The Makutani Palace” Msikiti Mkubwa “The Small Mosque”, Makaburi ya Shirazi “The Shirazi Tombs”, na Songo Mnara.
Mhandisi katika mradi huo Bw. Pierre Blanchard anasema kuwa ukarabati unafanywa kwa kutumia vitu asilia vilivyotumika awali katika ujenzi wa magofu hayo kama vile chokaa, udongo mwekundu, na mchanga.
Anasema kuwa iwapo ukarabati utatumia vifaa vya kisasa kama, cement, dhana nzima ya utunzaji wa magofu hayo itapotea kwa sababu haviendani na uhifadhi wake.
Ukarabati unafanywa na vijana 15 wa Kitanzania ambao wamepata mafunzo kutoka kwa watalaam wa kujitolea wa shirika lisilo la serikali la nchini Ufaransa liitwalo Chantiers, Histoire and Architecture Medievales (CHAM) linalojishughulisha na elimu ya utunzaji wa kumbukumbu za kihistoria, kazi mbalimbali za kujitolea kwa vijana katika uhifadhi na mafunzo kazini kwa wale wasiokuwa na ujuzi.
Lengo la CHAM ni kuwawezesha vijana hao kupata uelewa kuhusu utunzaji wa magofu kwani baadhi yao awali walikuwa ni wavuvi au wakulima na wengine ni wasichana ambao hawajashiriki katika ujenzi kabisa.
Meneja mradi anasema kuwa kitajengwa pia kituo cha kutoa habari ili kutoa taarifa kwa wageni na watu wengine watakaokuwa na kiu ya kujua zaidi kuhusu eneo hilo la magofu lililotangazwa kuwa urithi wa Dunia mwaka 1981.
Hii ni moja kati ya hatua nyingi za kuitambulisha historia ya Kilwa kitaifa na kimataifa, na ni muhimu kwani tayari baadhi ya wadadisi wamesema kuna hatari ya vitu vilivyopo na historia yake kupotea kabisa barani Afrika iwapo havitatunzwa vizuri.
Kilwa kama ilivyo baadhi ya miji katika mwambao wa bahari ya Hindi ulikuwa ni kituo kikubwa cha biashara katika karne ya 13 na 14 hivyo kuvuta wafanyabiashara kutoka kona mbalimbali duniani.
Mji huo wa kusini ndio pekee uliokuwa na sarafu yake katika ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara (Sub Sahara Africa). Katika kipindi hicho biashara nyingi ilifanywa kwa kubadilishana vito (barter trade).
Inasemekana kuwa ingawa mambo mengi ya kale yanapatikana barani Afrika, Tanzania ikiwa moja ya nchi zenye kumbukumbu za kitamaduni za kale, wengi miongoni mwa wakazi wa Afrika hawaelewi chochote au wana uelewa kidogo mno kuhusu kumbukumbu hizo ambazo zinawahusu.
Kilwa ndiyo iliyokuwa na msikiti mkubwa katika karne ya 11 na 15 ambao hadi leo upo uliotumika wakati wa sherehe ukikusanya watu kutoka kona zote za mwambao hadi Mombasa na Sofala. Kulikuwa na misikiti 99 katika kipindi hicho ambayo baadhi magofu yake bado yapo.
Wapo wanaodai kuwa sehemu za ukanda wa kusini katika utalii zimesahaulika kabisa. Hata hivyo serikali na wahisani mbalimbali wanaboresha maeneo hayo yawe ya kuvutia zaidi kwa watalii na wageni mbalimbali mara wafikapo hapa nchini au wakiwa nje ya nchi wawe na shauku ya kufika na kujionea hazina za mambo ya kale zinazopatikana katika sehemu hizo.
Mkuu wa wilaya ya Kilwa Bw. Bernad Itendele anasema kuwa wakazi wa eneo hilo wanafundishwa mambo mbalimbali ikiwamo namna ya kuwapokea watalii, kuwafunza utamaduni wao na kujifunza kutoka kwao bila woga.
Anasema kuwa wilaya hiyo imepata umaarufu katika utalii baada ya samaki aina ya Silicant zaidi ya miaka milioni 65 iliyopita kuvuliwa katika eneo hilo.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi wa wilaya ya Kilwa, Bw. Muhando Harold Senyagwa anasema Daraja la Mkapa limeleta mabadiliko mengi, ikiwamo idadi ya wageni kuongezeka kila kukicha na upatikanaji wa usafiri wa uhakika.
Pamoja na juhudi nzuri zinazofanywa na serikali kwa kuwashirikisha wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwamo utalii wa jamii, (community tourism) ili kuinua uchumi na hali za maisha, bado juhudi kubwa zaidi inahitajika ili kufikia viwango vinavyostahili hasa katika utalii ambao kila kukicha unakua kwa kasi ya ajabu.
Baadhi ya wakala wa watalii kutoka katika nchi za ulaya wana mtizamo kuwa bado huduma ya utalii inastahili kuboreshwa ili iendane na gharama zinazotozwa, ikiwa ni pamoja na wanaojishughulisha katika kazi za utalii kuwa na elimu kuhusu shughuli zao.
Takwimu za watalii waliofika nchini kati ya mwaka 1998-2002 zinaonyesha kuwa watalii kutoka Ulaya, wengi wanatoka katika nchi za Uingereza, nchi za Scandinavia, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Holland, na Uswisi.
Inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2012 wageni watakaoitembelea Tanzania watafikia idadi ya watu zaidi ya 900,000 ambapo idadi hiyo kubwa ya wageni watakaofika itachangia kuongeza kipato katika sekta nyingine za uchumi.
Idadi ya wageni inaongezeka kwa sababu ya mambo mengi ikiwamo utunzaji wa vivutio vinavyopatikana hapa nchini unaofanywa na serikali na wananchi kwa ujumla hasa wale wanaozunguka maeneno ya utalii.
Aidha, Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA) lilianzishwa mwaka 1959 pamoja na mambo mengine, kutunza hifadhi za Taifa ili zisivamiwe au kuharibiwa kwa namna yoyote kuwezesha wananchi na wageni mbalimbali kuzitembelea wakati wowote.
Kutokana na uhifadhi wa makini hasa wa maliasili Tanzania yenye eneo la kilometa za mraba 937,062 yaweza kujinadi kuwa ni moja kati ya nchi ambazo mtalii anaweza kufunga safari na kupumzika kwa kuangalia vivutio mbalimbali na kumbukumbu za zamani ambazo hazipatikani mahali pengine popote Duniani.
Katika kongamano la pili la Kimataifa la Afrika Kuhusu Nafasi ya Utalii Katika Kudumisha Amani lilofanyika hapa nchini Dr. Dawid De Villiers ambaye ni Katibu wa Shirika la Utalii la Dunia (WTO) aligusia kuwa bara la Afrika bado lina nafasi kubwa ya kufaidika na utalii, hata hivyo bado soko la sekta hiyo halijatumika ipasavyo kwa maendeleo katika jamii, bara la Afrika linawakilisha asilimia nne katika biashara ya dunia.
Alisema iko haja ya kuhakikisha picha mbaya inayolieleza bara la Afrika kama sehemu ya njaa, magonjwa na migogoro, ambapo wakati tatizo liko katika nchi moja au sehemu ndogo hali hiyo huchukuliwa iko katika bara lote.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Mkuu Mhe. Frederick Sumaye alisema kuwa tukio lolote la kigaidi linapotekea ndani au nje ya Afrika huleta picha mbaya hivyo kupunguza idadi ya watalii na wawekezaji wengine hivyo kudumuza uchumi. Takwimu zinaonyesha nchi 33 kati ya 48 masikini zipo katika bara la Afrika.
Ingawa bara la Afrika lina vivutio vingi ambavyo bado havijatumika kisawasawa kwa sababu ya matatizo mbalimbali, takwimu za WTO zinaonyesha kuwa sekta ya utalii inaingiza dola za Kimarekani (USD) trillioni 3.6 na kutoa ajira moja kati ya watu 12 duniani.
Hapa nchini, na nchi nyingine za Kiafrika utalii ni moja kati ya sekta zinazotegemewa katika kuingiza fedha za kigeni hivyo kuchangia kuondoa umaskini, ambao ni mkakati wa serikali ya Tanzania kwa kuwashirikisha wananchi kuondosha umasikini.
Hata hivyo, Raisi wa Shirikisho la Sekta Binafsi la Tanzania (TPSF) Elvis Musiba aliweka bayana kuwa sekta binafsi bado “imelala usingizi” kwa sababu ya ukubwa wa mtaji unaohitajika katika kuendesha sekta hiyo.
Aliongeza kuwa matumizi mabaya ya maliasili yataleta athari kwa utalii hivyo ni muhimu kwa wananchi katika sekta binafsi kuisadia serikali katika kupambana na wahalifu waharibifu wa maliasili ili kuleta utalii endelevu
Baadhi ya tafiti kuhusu maendeleo ya Afrika zinatilia shaka bara hilo kwamba haliko sambasamba na karne ya 21 ambapo kipato katika ukanda wa Sahara (Sub Sahara Afrika) kimekuwa kidogo kuliko ilivyokuwa mwishoni mwa miaka ya 1960.
Tafiti zinaonyesha kuwa kati ya Waafrika watano, mmoja yumo katika migogoro pamoja na hayo wale wenye ujuzi hukimbilia nchi za ng’ambo wakati idadi ya wakazi katika bara hilo imeongezeka mara mbili. Katika miaka 30 iliyopita.
Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa ukianza na ujenzi wa mlango wa nyasi hakika utabadilika na kumalizia kwa ujenzi wa mlango wa chuma, hivyo mradi wa ukarabati wa magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara utaleta maendeleo kwa wananchi.
mwisho

No comments:

Post a Comment